TAKUN · MWONGOZO

Mwongozo wa kutumia TAKUN

Mialiko, website za biashara na wasifu — hatua kwa hatua, kwa maneno rahisi.

Kazi yako inahifadhiwa kwenye akaunti yako. Ukiingia kwa simu au kompyuta nyingine, utaiona.
01

Kuanza: jisajili au ingia

Kuangalia miundo na mifano ni bure na hakuhitaji akaunti. Ili kutengeneza na kuhifadhi, jisajili kwa Google au kwa barua pepe na nenosiri jipya la TAKUN (herufi 8 au zaidi). Tutakutumia barua pepe ya kuthibitisha. Ukichagua muonekano kabla ya kuingia, utarudishwa kwenye muonekano huohuo baada ya kuingia.

02

Nenosiri na usalama

Tumia nenosiri la TAKUN pekee. Ukilisahau, bonyeza “Umesahau nenosiri?” na tutakutumia link ya kuweka jipya — hatuwezi kukuonyesha nenosiri la zamani. Ukikosea mara nyingi, utaombwa kusubiri kidogo. Ondoka (Log out) ukitumia kifaa cha mtu mwingine.

03

Kuchagua muonekano

Fungua Miundo, chagua Mialiko, Biashara au Wasifu, kisha gusa mfano kuuona wote kwa upana wa simu au kompyuta. Ukipenda mmoja, bonyeza “Tumia muonekano huu”. Unaweza kubadilisha baadaye bila kupoteza ulichoandika.

04

Kutengeneza mwaliko

Jaza aina na jina la sherehe, wenyeji ukipenda, tarehe (andika siku/mwezi/mwaka, mf. 25/12/2026), saa (saa za Tanzania), mahali, maelekezo mafupi, ujumbe, na namba mbili au tatu za wenyeji. Weka pia picha itakayoonekana kwenye mwaliko wako — mtu mmoja, wanandoa au kundi; unaweza kuisogeza na kuikuza ili kila mtu aonekane. Unaweza kuwa na sherehe mbili zinazoendelea kwa wakati mmoja.

05

Kuongeza wageni

Tunahitaji jina la mgeni tu na kama mwaliko ni wa mtu mmoja (Single) au watu wawili (Double). Ongeza mmoja mmoja, bandika orodha, au pakia CSV/XLSX. Kila sherehe ina nafasi za watu 1,000. Kila mwaliko unapata msimbo wake wa kipekee unaotengenezwa na TAKUN; haubadiliki ukibadilisha muonekano.

06

Kupakua na kutuma mialiko

Kabla ya kupakua, sherehe lazima iwe na picha. Pakua mwaliko mmoja kama picha (PNG 1080×1080) au PDF, au chagua mingi na upakue ZIP moja au PDF moja. Unaweza kusitisha wakati wowote; faili lisilokamilika halipakuliwi. Kisha tuma mwenyewe kwa WhatsApp au programu nyingine. Ukibadilisha taarifa za sherehe, pakua na utume upya.

07

Timu ya sherehe

Fungua Timu ya sherehe, nakili link ya timu na uitume kwa wasaidizi. Kila mmoja anaingia kwa akaunti yake, kisha wewe unamkubali kama Mpokeaji wa wageni au Msimamizi msaidizi. Unaweza kuondoa ruhusa wakati wowote — inaacha kufanya kazi mara moja. Wewe pamoja na wasaidizi 9 tu.

08

Kupokea wageni mlangoni

Fungua Kupokea wageni, chagua sherehe, kisha scan QR kwa kamera au andika msimbo. Utaona jina la mgeni na nafasi zilizobaki. Bonyeza “Thibitisha” ili aingie. Mwaliko wa watu wawili unaweza kuingiza mmoja sasa na mwingine baadaye. Ikiwa wasaidizi wawili watascan mwaliko mmoja kwa wakati mmoja, nafasi haitumiki mara mbili.

09

Ukikosea msimbo

Ukiandika msimbo usiotambuliwa, tutakuambia una majaribio mangapi yaliyobaki. Ukikosea mara 5 mfululizo, utasubiri dakika 5 — hii inakuhusu wewe tu kwenye sherehe hiyo. Msimbo sahihi unaanzisha hesabu upya. Mwaliko uliokwisha kutumika na tatizo la intaneti havihesabiwi kama kosa.

10

Website ya biashara

Weka jina la biashara, unachouza, mahali, saa za kazi, nembo na picha. Ongeza bidhaa au huduma hadi 10, kila moja na picha hadi 3 na bei kwa TZS au “Omba bei”. Kila bidhaa ina kitufe cha “Uliza kwa WhatsApp” kinachotumia namba YAKO. Hakuna kikapu wala malipo.

11

Wasifu wako

Jitambulishe, weka unachofanya, ujuzi wako, na kazi hadi 10 zenye picha hadi 3 na link. Andika ukweli tu.

12

Kuchapisha na link yako

Kazi yako inahifadhiwa kama rasimu ya faragha unapoandika. Chagua jina la link (mf. takun.willytechbro.tech/jina-lako) — kila jina ni la mtu mmoja tu, na baadhi kama admin au login yametengwa. Bonyeza “Chapisha” ili watu waone. Ukibadilisha baadaye, bonyeza “Sasisha ukurasa wa umma”. “Ondoa hewani” inazima link mara moja.

13

Baada ya sherehe

Siku 7 baada ya sherehe (saa za Tanzania), majina ya wageni, misimbo, rekodi za kuingia na picha ya sherehe zinafutwa. Utaona tarehe hiyo kwenye sherehe yako. Pakua orodha ya wageni kabla ya hapo ukiihitaji. Takwimu za jumla tu zinabaki. Mialiko uliyokwisha kutuma haiwezi kufutwa kwenye simu za watu.

14

Kazi uliyoanza kabla ya akaunti

Kama ulitengeneza kitu kwenye kifaa hiki kabla ya akaunti kuwepo, fungua Akaunti yangu na uchague “Hamishia akaunti”. Hatubadilishi kazi iliyo kwenye akaunti yako tayari. Mialiko iliyohamishwa inapata misimbo mipya, kwa hiyo pakua na utume upya.

15

Kupata msaada

WhatsApp +255619470497. Simu +255619470497 au +255746474232. Tunajibu kila siku 07:00–19:00 (saa za Tanzania). Ukurasa ukishindwa kufunguka: Angalia muunganisho wako wa intaneti, kisha jaribu tena.

Wasiliana nasi